Friday, 15 February 2013 07:08

Ujenzi wa mji mpya Kigamboni kubadilisha Jiji la Dar es Salaam

               Ujenzi wa mji mpya Kigamboni kubadilisha Jiji la Dar es Salaam
MPANGO wa kujenga mji mpya wa Kigamboni jijini Dar es Salaam ulianza rasmi mwaka 2008 na unatarajiwa kukamilika ifikapo mwaka 2032.

Moja ya sababu inayokwamisha kuanza kwa mradi huo ni ukosefu wa fedha unaotokana na bajeti finyu ya serikali.

Mradi huo  una malengo ya kibiashara, kwa mfano ramani ya mji huo inaonyesha kutakuwapo na shughuli za  utalii na kuboresha shughuli za kiuchumi na kijamii.

Serikali kwa upande wake imekuwa ikipanga mikakati mbalimbali ya kuanzisha mradi huo ikiwa ni pamoja na kulipa fidia kwa wananchi wa Kigamboni ambao wataondolewa katika eneo la mradi na kuhamishiwa eneo lingine la Kigamboni.

Hata hivyo, pamoja na serikali kuwa na mipango hiyo wananchi wa Kigamboni wamekuwa wakipinga kuwapo kwa mji huo kwa kuhofia kudhulumiwa na kutokulipwa fidia stahili.

Serikali kwa kuonyesha umuhimu wa mradi huo imeanzisha Wakala wa Kuendeleza mji wa Kigamboni (KDA) ili kusimamia na kuendeleza mji huo pamoja na shughuli nyingine.

Hivi karibuni Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, Profesa Anna Tibaijuka ametangaza kuanzishwa kwa Wakala  huyo.

Mji mpaya Kigamboni utajitegemea

Mji wa Kigamboni utakuwa mji unaojitegemea bila kutegemea usimamizi  kutoka Manispaa ya Temeke.

Profesa Tibaijuka anaesema Serikali imeamua kufanya hivyo  ili KDA  ipange na kusimamia ujenzi wa mji huo wa kisasa.

“KDA imeanzishwa chini ya Sheria ya Wakala wa Serikali ya 1997 kwa lengo  kujenga mji huo katika ubora uliokusudiwa,”anasema Profesa Tibaijuka.

Anasema baada ya kuanzishwa kwa KDA, kata zote za Kigamboni zitaungana na madiwani wa kata hizo akiwamo mbunge  watakutana katika baraza la ushauri la KDA.

“Kutakuwa na Baraza la Kigamboni ambalo madiwani na mbunge wao watajadili maendeleo ya mji huo na leo (jana) kutakuwa na kikao cha kwanza,”anasema Profesa Tibaijuka.

Kata ambazo zitaungana ni Kigamboni, Tungi, Mjimwema,Vijibweni, Kibada, Pemba Mnazi, Kimbiji, Kisarawe II, Somangila, Kendwa, Sinda Chini na Sinda Juu.

Profesa Tibaijuka anasema eneo lote la Kigamboni lenye Hekta 50,935 litaendelezwa na wananchi 80,000 wa eneo hilo watanufaika.

Profesa Tibaijuka anasema wananchi wa Kigamboni ambao wako kwenye maeneo ambayo yatahitajika kwa ajili ya ujenzi huo watashirikishwa katika mchakato na kulipwa fidia kwa wakati. Anasema zaidi ya Sh11 trilioni zitatumika kujenga mji huo.

“Bajeti ya mwaka huu tulihitaji Sh600 bilioni, lakini tukapewa asilimia 10 ya fedha hizo ambayo ni Sh60 bilioni, tunajipanga na hii ni moja ya mipango yetu ya kufanikisha ujenzi huo.

“Katika awamu ya kwanza tutahitaji Sh 3 trilioni ili kuifanikisha ujenzi huo.” anasema Profesa Tibaijuka.

Mbunge wa Jimbo la Kigamboni, Dk Faustine Ndugulile anaonekana kupinga kuwapo kwa KDA kwa sababu  mpango huo unaongeza gharama kwa serikali.

Dk Ndugulile anasema Manispaa ya Temeke iwezeshwe ili kusimamia mji huo.

“Walikuja kutueleza hilo suala, lakini sisi na Manispaa tulikataa kwa kuwa manispaa ina uwezo wa kufanya kazi hiyo hivyo hatukubaliani na  mamlaka hiyo,”anasema Dk Ndugulile.

Faida za ujenzi wa mji huo

Septemba 20 mwaka jana, Rais Jakaya Kikwete akizindua ujenzi wa Daraja la Kigamboni alisema daraja hilo litachochea kasi ya ujenzi wa Mji mpya wa Kisasa wa Kigamboni.

“Mji huu utasaidia sana kufungua fursa za uwekezaji katika eneo hilo na kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijamii kwa wakazi wa Dar es Salaam na wananchi wote kwa ujumla. Tunategemea watu watawekeza kwenye viwanda, hoteli, migahawa, nyumba za makazi na biashara. Hivyo vijana wetu watapata fursa mbalimbali za ajira na shughuli nyingine za kujiongezea kipato,”anasema Rais Kikwete.

Rais Kikwete anasema vilevile Mji mpya wa Kigamboni utasaidia kupunguza tatizo la uhaba wa makazi bora na ujenzi holela ambalo linasababishwa na kasi kubwa ya ongezeko la watu Jijini Dar es Salaam kuliko idadi ya viwanja vya makazi vinavyopimwa au nyumba zinazojengwa.
 
“Mji mpya wa Kigamboni utakapokamilika utaongeza makazi ya watu kutoka 45,000 waliopo sasa mpaka 450,000,”anasema Rais Kikwete.

Wapinga wakala kusimamia Mji wa Kigamboni.

Mbali na kutajwa kwa faida ya kujengwa kwa mji huo, wakazi wa Kigamboni, wamelalamikia kuwapo kwa siri kubwa katika Wizara ya Ardhi, Nyumba na Makazi kwenye mchakato wa kumtafuta Wakala wa Kuendeleza mji wa Kigamboni (KDA) pamoja na ujenzi wa mji huo.

Malalamiko hayo yamekuja baada ya Waziri, Profesa Tibaijuka kuanzisha wakala atakayesimamia maendeleo ya ujenzi wa Mji mpya wa Kigamboni na kujitegemea badala ya kusimamiwa na Manispaa ya Temeke.

Baadhi ya wakazi wa Dar es salaam kwa nyakati tofauti wamesema wana hofu na hatma ya masilahi yao kwa kuwa mchakato wa ujenzi wa mji huo umekuwa ukifanwa kwa siri bila wananchi kushirikishwa katika hatua za awali.

Wamesema hawapingi uamuzi wa Serikali kujenga mji huo bali wanapinga kitendo cha serikali kutowashirikisha wananchi wakati wa kufanya maamuzi.

Mwenyekiti wa Mtaa wa, Feri Juma Mihambo anasema ujenzi wa mradi huo umekua ukisuasua tangu mwaka 2008, lakini walishtushwa na taarifa za kuanzishwa kwa wakala  kutoka kwenye vyombo vya habari kwamba ni chombo kitakachosimamia mji wa Kigamboni.

“Serikali  inapaswa kukaa meza moja na wananchi na kuwaeleza kwa kina kwanini mradi umechelewa kwa takriban miaka minne na pia kwanini imefanya siri kuanzisha wakala ambaye atashirikiana nao bila wao kujua,” anasisitiza Mihambo.

Naye Nassoro Chano anasema wakala asimamie mpango mji pekee na kuwaachia wananchi uhuru wa kukubaliana na wawekezaji katika masuala ya viwanja na mali nyingine.

“KDA ituachie jukumu la kuingia ubia na mwekezaji ili tupate masilahi stahiki na mwekezaji huyo atatakiwa kujenga kwa kufuata mipango na ramani iliyotolewa na wakala,” anasema Chano.

Mkazi wa Kigamboni, Ngoroka Ngoroka anasema serikali iwafuate wananchi na izungumze nao upya kuhusu mradi huo, kwa kuwa siyo busara kupokea maamuzi kutoka ngazi za juu.

Titus Lugoe anasema serikali iache tabia ya kukurupuka na kuwalazimisha wananchi kuwa wapokeaji wa taarifa na maamuzi wakati wao ni wadau muhimu wa kufanikisha mipango ya serikali.

“Mwaka 2008 tulitangaziwa tusiendelee na ujenzi wa miradi yetu, lakini baada ya hapo hakuna kilichoendelea mpaka tulivyosikia kwenye vyombo vya habari kuwa mradi unaendelea,” anashangaa!

Anasema kuwa kuwa serikali imekuwa haiwashirikishi, wananchi wamekuwa wakiishi kwa mashaka na wana hofu ya   kupata maslahi stahiki wakati wakihamishwa ili kupisha mradi wa ujenzi huo.

Read 2023 times